Thursday, August 26, 2010

Waandishi Kagera waanza ucgunguzi kwenye kata 30

Kufuatia waandishi wa Habari mkoani kagera,kupata fedha kutoka TMF sasa wameanza rasmi uchunguzi kutafuta chanzo cha wananchi katika wilaya ya Bukoba kutojiandikisha kwa wingi kupiga kura na hata wachache wanaojiandikisha kutojitokeza kwa wingi kupiga kura

Uongozi KPC unawatakia kazi njema

Monday, August 16, 2010

Tahariri ya Gazeti Malengo Yetu Toleo No 14

Kauli hizi za wanasiasa wanawake hazifai !

Wakati tunaunga mkono harakati za kutafuta usawa wa kijinsia zinazofanywa na Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, wanaharakati, wanawake wenyewe pamoja na sisi wanaume, katu hatuungi mkono fikra zinazopandikizwa sasa kuwa wanawake ni lazima kuwachagua wanawake wenzao.

Katika awamu hii ya uongozi wa nchi unaokaribia kumaliza muda wake ukiahidi kuwa lengo lake kuhusu wanawake ni kuwa wawe asilimia hamsini kwenye vyombo vya maamuzi zinaenezwa fikra potofu zinazoashiria kuchochea hisia za ubaguzi na mapambano ya wanawake dhidi ya wanaume.

Kuwa wanawake wako upande wao halikadhalika wanaume upande wao hali inayoashiria kujenga matabaka katika nchi yetu. Hali hii haiwezi kupewa nafasi na kuachiliwa iendelee kwa kuwa itakuwa inapotosha dhana nzima ya kuwawezesha wanawake na badala yake kuifedhehesha jamii nzima.

Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wapiga kura waelimishwe kumchagua kiongozi mwadilifu, anayeelewa matatizo yao, mwenye maono na ambaye ni sehemu ya jamii (‘anayekula na kuishi nao’kwa kila hali), lakini si kupiga debe achaguliwe fulani kwa sababu ya jinsi yake , kabila lake au dini yake.

Kwa hiyo tuwahamasishe wananchi wawachague viongozi bora na si kwa tofauti zao za kidini, kikabila wala kimaumbile. Hivyo yeyote atakayehamasisha watu kuwachagua wagombea kwa sababu ni wanawake na tofauti na yule anayepandikiza ubaguzi wa kidini au kikabila.

Kauli kama hizi ni maarufu sana katika kampeini ambazo tumeshuhudia hivi karibuni na hasa wakati wa kura za maoni za kuwatafuta wagombea wa vyama vya siasa. Mara utasikia, zinazotolewa kauli kwamba wanawake ni wenye huruma (kinyume chake wanaume ni wakatili ) wanawake wana upendo (wanaume wamejaa chuki ), wanawake ni waaminifu (wanaume si waaminifu)n.k.

Ni mtazamo wetu kuwa kama ilivyo kwa baadhi ya wanaume, hata katika kundi la wanawake kuna wasio na upendo, wasio waaminifu, wakatili na hata majambazi. Ndiyo maana tunawasihi watanzania tumchague kiongozi kwa kuangalia uwezo na zifa alizonazo mgombea kama kiongozi bora bila kutanguliza jinsi, kuwapa nafasi wanawake kuchukuliwa kuwa ni vita au uadui kati ya wanawake na wanaume.

Kama wanawake wote wataungana kuwaunga mkono wanawake wenzao tu,mwanaume gani atapita?.

Baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wanawake walishawahi kutoa kauli za kuchefua hivi karibuni mfano, mmoja wapo ni kiongozi mmoja wa wanawake aliyekaririwa katika chombo kimoja cha habari akisema ‘’Rafiki wa mwanamke ni mwanamke’’.

Baada ya siku chache kiongozi mmoja mwanamke akiwa kwenye ziara mkoani Arusha alikaririwa akiwataka wanawake kuwa na umoja na kupendana ili waweze kuwashinda wanaume katika uchaguzi mkuu.

Haitoshi mwingine akiwa wilayani Arumeru alikaririwa na vyombo vya habari akisema, ‘’Wanawake ni jeshi kubwa wakishirikiana wanaweza kuwania na kugombea nafasi mbalimbali na kuwashinda wanaume’’.

Hofu yetu sisi Malengo Yetu ni kuwa kutokana na uwingi wa wanawake tutakuwa na bunge la wanawake, endapo kauli kama hizo za viongozi maarufu na wenye ushawishi katika jamii zitaachwa kuendelea kutolewa. Kwa hali kama hiyo lengo la 50 kwa 50 halitawezekana.

Hata hivyo hatari nyingine inayoonekana ni kuwa sasa kuna kundi moja katika jamii ambalo limejipanga kuanzisha mapambano. Sasa hofu yetu inajengeka katika ukweli kuwa ni athari gani zinazoweza kujitokeza endapo kundi linaloshambuliwa katika jamii wakati wa mapambano hayo litaamua kujihami?

Pengine sio rahisi kupata jibu. Sisi Malengo Yetu tunaamini kuwa mchakato kufikia malengo ya asilimia 50 kwa 50 za wanawake na wanaume katika nafasi za maamuzi hatuhitaji kutumia lugha za kuchochea mapambano bali kutumia uhamasishaji. Wengine katika lugha sanifu zaidi wanasema tunahitaji kutumia uzengeaji na uchechemuzi( lobbying and advocacy).

Katika matumizi mabaya ya Demokrasia ipo mifano ya maamuzi ya ovyo yaliyofikiwa na kuwa na athari mbaya kwa jamii kutokana na kutumia kigezo cha wengi wape. Kwamba hata kama wale wachache walikuwa na mawazo ya kufikiwa kwa maamuzi ya busara basi kwa kigezo cha upigaji kura wengi wenye maamuzi ya ovyo wakapata kura nyingi na uamuzi wao kuwa ndio utakaotumika kwa kigezo cha Demokrasia.

Katika maana yake halisi Demokrasia ni kama mkondo wa maji mbayo hutiririka siku zote kutoka kileleni hadi bondeni, maji hayawezi yenyewe kupanda kilele cha mlima hadi nguvu fulani itumike.

Kwa hiyo demokrasia ya wanawake kushika nafasi za uamuzi kwa asilimia 50 kwa 50 inabidi itumike kwa busara katika uchaguzi ujao. Isije kuwa kulazimisha maji kupanda kilele cha mlima. Lengo la uchaguzi si wanawake kuwashinda wanaume bali ni kushindanisha hoja, fikira,mitazamo,maono na uwezo wa kuwa kiongozi bora wa wanaume, wanawake na watoto.