Tuesday, September 7, 2010

Huyu 'Muhuni" kwenye msafara wa Kikwete analipwa na nani

Na Antony Mayunga

NDEGE wa aina moja huruka kwa pamoja ,ni msemo wa wahenga wetu waliotutangulia,wakimaanisha watu wa itikadi moja hufanya mambo yao kwa pamoja.

Lakini msemo huo unakuwa kinyume kwa viongozi na wanachama wa baadhi ya vyama vya siasa kutokana na kampeni za uchaguzi mkuu unaoendelea kutawaliwa na vibweka vingi .

Miongoni mwao ni kauli ya iliyotolewa na Katibu wa CCM Taifa Yusuph Makamba kuhusiana taarifa kuwa kuna baadhi ya waandishi wa Habari walizuiwa kushiriki katika msafara wa Mgombea urais kupitia CCM

Makamba alikaririwa na vyombo vya Habari akidai kuwa mtu aliyefanya hivyo ni mhuni mmoja bila kumtaja jina.

“Huyo si uamuzi wa Chama ,ili uwe wa chama lazima uafikiwe na kamati kuu,Nec au uamzi afanye Katibu mkuu,vikao hivi havikufanyika kokote na mimi
katibu mkuu sijaagiza mtu awafukuze waandishi,fuatilia vizuri habari yako utagundua kuwa yupo mhuni amekosana nao akawafukuza,”mwisho wa kumnukuu Makamba wakati akihojiwa na gazeti la kila siku la Mwananchi.

Mimi nikiwa Mwandishi wa Habari kauli hiyo inanipa mashaka juu ya umakini wa chama hicho kikongwe
kuwa na ‘mhuni’ mmoja katika timu yao ya kampeini ambaye anaweza kuamua kuwafukuza waandishi harafu wakaishia kumkandia huku akiendelea na uratibu.

Kwa mjibu wa kamusi mhuni ni Mwanamme ambaye hajaoa,kapera,mseja,mtu asiyekuwa na mahali maalum pa kuishi,mwizi ,mvunjaji
sheria,mnyang’anyi,mchopozi.

Kama maana ni hiyo Makamba anataka kuwaambia wanachama wake kuwa wamekosa watu makini mpaka wakachukua watu wa namna hiyo.


Anataka watanzania waamini kuwa Mgombea Urais wa CCM katika timu ya kampeini ya mgombea huyo kuna baadhi ya watu ambao ni wavunjaji wa sheria,wasiojulikana makazi yao.

Hivi kweli mhuni ambaye hajulikani anawezaje kupewa jukumu kubwa kama hilo na akaharibu wakaishia kudai ni mhuni mmoja bila kuchukua hatua,hii si ni danganya toto?
Kama ni kweli ‘mhuni’ huyo aliwafukuza waandishi kwenye msafara wa Kikwete ataachwa aendelee na kuratibu kazi za wasiokuwa wahuni, tutaraji nini.

Hivi watazinduka siku akimfukuza kiongozi wa CCM kwenye msafara ,na ni nani anamlipa mhuni huyo kwa kuzunguka na msafara huo?.

Inawezekanaje mhuni akapewa kitengo kizito cha kuamua mwandishi gani ashiriki msafara na nani abaki.

Je kwa kauli hiyo inamaanisha nani alimchagua na alipewaje nafasi hiyo ili hali wakijuakuwa
ni mhuni.

Nadhani ipo haja ya kutueleza jina kamili la mhuni huyo kwani Makamba alidhani kwa kusema hivyo kunatosha kuwaridhisha wananchi kuwa chama kimesikitishwa na kitendo hicho haramu.

Kwa kweli hizo ni porojo ambazo kwa zama hizi hazitakiwi kuvumiliwa maana kwa kufanya hivyo ,inatia shaka juu ya utendaji wa chama hicho kinachojigamba kila kukicha kuwa ni makini .

Maana huwezi kupata chama makini bila kuwa na watendaji makini,kwanza.

Kwanini uhuru wa waandishi uingiliwe, na kwa maslahi ya nani.

Katika katiba ya Jamhuriya Muungano ya mwaka 1977 ibara ya18(d),kifungu hiki kinampa haki mwananchi ya kupewa taarifa mbalimbali muhimu kuhusu maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala
muhimu kwa jamii na watu wa kufanya kazi hii ni waandishi wa Habari kama waliofukuzwa.

Hivyo kwa chama makini kukaa kimya kwa mtu kuvunja katiba ibara hiyo kwa kifungu (b)na (c)kwa waandishi wa habari,inawapa mashaka watanzania wanaotaraji kufanya maamzi yao sahihi oktoba 31 .

Maana kwa kuwazuia waandishi kulikuwa na agenda ya siri isiyotakiwa kujulishwa jamii,ambayo inahitaji taarifa nani anafanya nini na wapi ,na anamkakati wa kuwafanyia nini watanzania.

Hivyo kumwachia “mhuni” rungu ya kubagua waandishi katika kampeini za Kikwete ni hatari sana.

Aidha waandishi wanaoandamana na wagombea waanchu ushabiki,kuvaa sare za vyama kwani hivyo ni kinyume na maadili ya taaluma.

Kwa kuacha hulka hizo watatenda kazi zao wakiwa huru,bila kuvalishwa nguo za chama ,na hayo ndiyo matarajio ya jamii kwa kipindi hiki ambacho
wanahitaji uchambuzi wa kina wa sera ,ilani na mikakati ya vyama vyote na wala si ushabiki.

Mwandishi anapatikana kwa simu no 0787239480.

Makala hii imetolewa kwenye gazeti Malengo Yetu Toleo la leo septemba 7,2010

No comments:

Post a Comment