Tuesday, September 7, 2010

Mapungufu kwa wagombea wote haya hapa !


Na Mwandishi Wetu.
Harakati za kampeni zikiwa zimepamba moto kwa wagombea wa nafasi za Urais,Ubunge na Udiwani tayari kumejitokeza mapungufu makubwa ambayo iwapo hayatarekebishwa yanaweza kuathiri mantiki nzima ya mchakato wa uchaguzi Mkuu.
Aidha imebainika kuwa hakuna chombo chochote kinachoratibu kampeini za wagombea kubaini kama wanayoyafanya kwenye kampeini zao ni sawa au wafanye marekebisho.
Uchunguzi wa gazeti hili tangu kuanza rasmi kwa kampeini hizo August 20 mwaka huu umebaini kuwa wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge wanafanya kampeini ambazo hazitoi nafasi kwa wapiga kura kuwapima.
Hivyo hivyo wagombea nafasi za Urais wakiwemo Mutamwega Mutahywa(TLP),Hashimu Rungwe (NCCR-Mageuzi),Ibrahimu Lipumba,Willbroad Slaa(CHADEMA) na Jakaya Kikwete(CCM) ambao tayari wamezindua kampeini zao nao wamekumbwa na ‘ugonjwa huo’.
Kwa mjibu wa Uchunguzi huo ni kuwa kati ya wagombea hao hakuna hata mmoja anayetoa fursa za kuulizwa maswali au kuwataka wasikilizaji kupata ufafanuzi wa jambo lolote.
Imebanika kuwa wagombea wote wamekuwa wakihutubia tu na baada ya mkutano kuondoka huku wakiacha maswali mengi kwa wapiga kura ambao hukosa fursa ya kujua hasa mgombea alichosema .Na wanaotaka kupata ufafanuzi wa jambo lililosemwa huachwa njia panda
Mathalan,mgombea anasema kuwa iwapo atachaguliwa atahakikisha nchi inaondokana na umaskini kwa muda wa siku 100 lakini hatoi nafasi kwa wananchi kuuliza jambo juu ya hoja zake hizo.
Wapiga kura waliohojiwa walisema kuwa hawaoni haja ya kwenda kwenye mikutano ya kampeini kwani inakuwa kama wanapata hotuba zilizorekodiwa kupitia kwenye redio au Television.
Uchunguzi umebaini kuwa hata katika ratiba zao hakuna kipengele cha maswali bali kuna muda wa wagombea kuongea na wananchi na siyo kueleza sera zao.
“Wote hawataki tuwaulize maswali na wanatoi ahadi ambazo hata hazitekelezeki na wengine walishindwa kutekeleza kwa kipindi cha nyuma lakini kwa kuwa hawatoa fursa ya maswali wanatulisha sera zao tu na kuondoka”Alisema Bw Theresphory Maiko mkazi wa Rwamishenye Bukoba mjini.
Akihojiwa na gazeti hili Mwanasheria wa kituo cha Sheria na Haki za binadamu(LHRC) cha Jijini Dar Es Salaam Pasience Mlowe ni kuwa hayo ni mapungufu makubwa kikatiba.
Mlowe anasema kuwa iwapo wananchi hawapati fursa hivyo ni vigumu kuwapima wagombea kwani na kwamba hii inaweza kuathiri mchakato wa kampeini kwao wengine wanaweza kudhani ndiyo utaratibu kumbe siyo.
“Ni haki ya wananchi kikatiba,wananchi kuhoji mgombea juu ya jambo lolote alilosema kwenye mkutano au kupata ufafanuzi wa jambo hilo na kinyume chake ni makosa hivyo ni wajibu wa wananchi kudai haki hiyo” Alisema.
Kwa upande wake Rais wa Shirika la People Organization Transparency Agency(POTA) Idrisa Masalu ni kuwa hotuba zinazotolewa katika mikutano ya hadhara ni lazima wananchi wapate fursa ya kuuliza maswali.
“Hii ni hasara kwa wagombea na wapiga kura kwani bila maswali,mgombea atapataje uhakika kama wapiga kura wameelewa na mpiga kura atajuaje kama anachosema mgombea ni sahihi”Alisema Masalu na kuongeza
“Sera siyo biblia,ni lazima mgombea aulizwe na ukiona anayekataa kufanya hivyo ujue hajiamini na anaogopa kuumbuka na kwa lugha nyepesi anapiga propanganda tu aelezi sera”.
Mbali na kasoro za kutokubali kuulizwa maswali pia imeibuka tabia ya baadhi ya wagombea kutoa ahadi zisizo tekelezeka na baadhi yao kufanya kampeini za matusi badala ya kueleza sera zao.
Mathalan,katika mikutano ya kampeini za CHADEMA,CUF na CCM ambazo zimefanyika katika uwanja wa mafumbo(CHADEMA),uwanja wa Uhuru(CUF na CCM) wagombea wamebanika kujadili mienendo ya wagombea wa vyama vingine tofauti na kueleza sera zao.
Wagombea hao wanatumia dakika 28 kati ya 30 walizopewa kutukana,kueleza sifa mbaya za wagombea wa vyama vingine,kutoa taarifa zisizo na udhibitisho juu ya wenzao,uzuri wa chama chao na dakika mbili au tatu ndizo wanazotumia kueleza sera na nini watawafanyia wananchi iwapo watachaguliwa.
Aidha imegundulika pia kwenye ajenda za kujadili kwenye mikutano hiyo ya vyama zimo ajenda za kujadili wagombea wa vyama tofauti na vyao
Baadhi ya wanachama wa vyama vya siasa vya CHADEMA,CUF na CCM walihojiwa juu ya kasoro hizo katika kampeini wengi walionekana kutojua faida wala madhara yake huku wengine wakionekana kuwa nas jazba kwa kudai kuwa muuliza swali ametumwa na wapinzani wao.
Hakuna kiongozi yoyote wa Vyama hivyo ngazi ya mkoa aliyekuwa tayari kutoa ufafanuzi juu ya kasoro hizo kwa madai wao wanajua mbinu za kutumia wakati wa kampeini.
Aidha Jeshi la polisi nchini limenoa askari wake na kuwapatia mavazi na vifaa vipya kama wanavyoonekana pichani mbele mahususi kwa ajili ya kudhibiti vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi kwa nchi nzima


Hii ndiyo habari kubwa kwa gazeti Malengo Yetu Toleo la leo Septemba 7,2010

No comments:

Post a Comment