Friday, January 22, 2010

Ni kweli Uchumi wa wanahabari Nchini Tanzania u mikononi mwa wahariri

Na Gordon Kalulunga

TASNIA ya habari ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine ingawa tofauti yake moja kubwa ni kwamba iko karibu zaidi na wananchi.

Vyombo vya habari vimekuwa vikiibua mijadala mingi kupitia makala mbalimbali. Si wote wangependa mijadala hiyo kuibuliwa kwa kuwa inawagusa.

Lakini pamoja na vyombo vya habari kuwa na nguvu hiyo, waandishi wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali.

Kuna matukio mengi yanayowakumba waandishi nchini na duniani kwa ujumla na hivyo wengi kuogopa kufanyiwa unyama kama walivyowahi kutendewa wenzao.

Hapa nataka kuweka wazi kuwa kuna waandishi wa habari wengi ambao wamekufa hapa nchini na vifo vyao havielezeki kutokana na ama kuuliwa kikatili au kuuliwa kibaiolojia. Lakini pia baadhi kulundikwa kwenye mahabusu za polisi kwa visingizio vya sheria.

Hali ya namna hii inawatia hofu waandishi wengi hasa yanapotokea matukio ya kutisha ya namna hii kama lile lililotokea mkoa wa Mbeya ambako mwandishi John Lubungo amekufa na kifo chake kimeacha maswali mengi yasiyo na majibu kwa wanahabari wenyewe na wadau wengine wa habari hapa nchini.

John Lubungo alikuwa Mtangazaji wa ITV; alifariki akiwa na umri wa miaka 34 siku ya Ijumaa ya Januari 25, 2008 majira ya saa 5.00 usiku akiwa anaendesha gari dogo akitokea mjini Mbeya akielekea Tunduma, wilayani Mbozi, mkoa wa Mbeya yalikoweko makazi yake.

Nikimnukuu aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Mbozi, Halima Kihemba, aliyesema kwa masikitiko: “Lubungo alikuwa mtu wa karibu sana na serikali na alipigania sana maendeleo ya mji wa Tunduma, wilaya ya Mbozi na mkoa kwa ujumla; na hapa nimetumwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, kuweka shada la maua kama ishara ya pole kwa familia na ndugu wengine.”

Naye aliyekuwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya, wakati huo, Suleiman Kova, ambaye ni mdau mkubwa wa wanahabari nchini, alisema alisikitishwa sana na kifo cha John Lubungo ambapo alimtaja John Lubungo kuwa mmoja wa waandishi ambao walikuwa wakiutetea na kuutangaza mkoa wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani hapa kwa kipindi hicho, Christopher Nyenyembe, alisema kuwa kifo cha mwanahabari huyo kilitokea ghafla na kilileta mshtuko mkubwa kwa taaluma ya wanahabari na wadau wote waliokuwa wakishirikiana vyema na marehemu katika uhai wake.

Si hayo tu bali hata ofisi aliyokuwa akiitumikia wakati wa uhai wake ilitoa masikitiko makubwa sana kwa kumpoteza kati ya makamanda wake wa kampuni lakini cha ajabu licha ya kusikitika kote huko likaibuka sula moja nyeti kuwa mwandishi huyo hakuwa na mkataba na kampuni hiyo!

Jambo hilo halikuwashangaza waandishi wengi bali lilisikitisha sana kutokana na kumjua vema marehemu Lubungo wakati wa uhai wake hasa uchapaji kazi wake wa muda mrefu katika chombo chake.

Sina nia ya kumwelezea binafsi ndugu yetu huyo aliyetangulia mbele ya haki lakini nia ya makala hii ni kuweka bayana mateso wayapatayo waandishi wa habari hapa nchini hasa waandishi wa mikoani.

Moja ya kero kubwa kwa waandishi hao hasa wa mikoani ni malipo kidogo wanayoyapata kutoka kwenye vyombo vyao vya habari wanavyovifanyia kazi na kutopewa mikataba kama sheria za kazi za nchi zinavyoelekeza.

Suala hilo limezua kansa ya manug’uniko kwa waandishi wa habari kutokana na kutoweza kutafutiwa ufumbuzi wala mjadala wa kitaifa jambo ambalo linatafsiriwa na baadhi yao kuwa ni kuvunja haki za binadamu na kiraia.

Mmoja wa waandishi ambao wamelaani vikali suala la mapunjo ya malipo kwa waandishi wa habari hapa nchini ni Mkurugenzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari (MIJO) kilichoko mkoani Mbeya, Jonas Mwasumbi.

Katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima kuhusu suluhisho la malalamiko ya muda mrefu ya waandishi wa habari juu ya malipo madogo wanayoyapata kutoka kwenye vyombo vyao wanavyofanyia kazi, alisema kuwa umefika wakati wahariri wa vyombo vya habari kubadilika kifikra na kimtazamo na waandishi wenyewe kujiendeleza zaidi kitaaluma.

Mwasumbi ambaye ni mwandishi mwandamizi wa magazeti ya Serikali hapa nchini na kiongozi wa muda mrefu wa MISA na taasisi nyeti za habari alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa na linatokana na waandishi wenyewe na baadhi ya wahariri wao.

“Malalamiko hayo yanatokana na elimu ndogo waliyonayo baadhi ya waandishi ambayo haimwezeshi mwandishi kupata ajira na baadhi hawafahamu haki zao za msingi juu ya ajira.”

“Pamoja na hilo tatizo, lingine liko kwa wahariri ambao hawana utu wala dini na kuendelea kuwanyonya waandhishi wao hasa wa mikoani huku wakiendelea kutumia kwenye magazeti yao habari za waandishi hao ambao hawawalipi ipasavyo jambo ambalo ni dhambi mbaya sana,” alisema Mwasumbi.

Mkurugenzi huyo aliendelea kueleza kwamba wahariri wa vyombo mbalimbali hapa nchini wanapaswa kubadilika na kuheshimu haki za binadamu; vilevile kwa upande wa waandishi wa habari wanapaswa kuongeza viwango vyao vya elimu ili kupambana na utandawazi na soko la ajira kwa ujumla hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa mtazamo wangu na kutokana na malalamiko ya waandishi wa habari hapa nchini ni muhimu ikaibuliwa hoja na mjadala stahiki juu ya mustakabali wa waandishi wa habari Tanzania ili kutambua dhana nzima ya utawala bora kwa viongozi wetu waliokabidhiwa dhamana na kuwawezesha waandishi wa nchi hii kukabiliana na hali mbaya ya kiuchumi inayowakabili.

Pamoja na kuibua hoja ya maslahi ya waandishi wa habari hapa nchini, pia mjadala ulenge kutambua na kuthamini kivitendo si kinadhalia thamani ya waandishi wa habari katika taifa hili ili kujua mustakabali wa waandishi wa habari wa Tanzania.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.


Imetolewa kwenye gazeti la Tanzania Daima Toleo la januari 19,2010

unaweza kuisoma kwa kuki click hapa

kazi njema.

No comments:

Post a Comment